30/03/2024
DOMINIKA YA PASAKA KATIKA UFUFUKO WA BWANA, MACHI 31, 2024
RANGI YA KILITURJIA: NYEUPE 🤍
SOMO LA KWANZA
MATENDO YA MITUME 10:34a, 37—43
Tulikula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuka kwake katika wafu.
Somo katika kitabu cha Matendo ya Mitume
Siku zile: Petro alifumbua kinywa, akasema, “Mmejua yaliyotukia katika Uyahudi wote kuanzia Galilaya baada ya ubatizo aliohubiri Yohane, jinsi Mungu alivyompaka mafuta Yesu wa Nazareti kwa Roho Mtakatifu na nguvu. Na jinsi alivyozunguka katika nchi yote akitenda mema na kuwaponya wote walioonewa na Shetani, kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye. Nasi ni mashahidi wa yote aliyoyafanya katika nchi ya Wayahudi na katika Yerusalemu. Naye walimtundika mtini na kumwua. Mungu lakini alimfufua siku ya tatu na kumjalia aonekane, si kwa watu wote, ila kwa mashahidi waliokuwa wamechahuliwa na Mungu, ndio sisi tuliokula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuka kwake katika wafu. Ndio sisi alituagiza yuwahubirie na kuwashuhudia watu kwamba: huyu ndiye aliyewekwa na Mungu kuwahukumu wazima na wafu. Huyu manabii wote wameshuhudia, kwamba kila anayemsadiki anaondolewa dhambi kwa jina lake.”
NENO LA BWANA… TUMSHUKURU MUNGU
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 118:1—2, 16ab—17, 22—23 (K. 24)
K. Hii ndiyo siku aliyofanya Bwana; tuishangilie na kuifurahia.
au: Aleluya
Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema,
kwa maana wema wake ni wa milele.
Israeli na aseme sasa:
wema wake ni wa milele. K.
Mkono wa kuume wa Bwana umetukuzwa;
mkono wa kuume wa Bwana umetenda makuu.
Sitakufa, bali nitaishi,
nami nitayasimulia matendo ya Bwana. K.
Jiwe walilokataa waashi
limekuwa jiwe kuu la pembeni.
Jambo hili alilifanya Bwana;
nalo ni la ajabu machoni petu. K.
SOMO LA PILI
WAKOLOSAI 3:1—4
Yatafuteni yaliyoa juu anakokaa Kristo.
Somo katika barua ya Mtakatifu Paulo kwa Wakolosai
Ndugu zangu: Ikiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu anakokaa Kristo kuume kwa Mungu. Zingatieni yaliyo juu, si mambo ya duniani. Maana mmekwisha kufa, na uzima wenu umefichika pamoja na Kristo katika utukufu. Baadaye Kristo aliye uzima wetu atakapotokea, ninyi pia mtatokea pamoja naye katika utukufu.
NENO LA BWANA… TUMSHUKURU MUNGU
Au lifuatalo:
SOMO LA PILI
1 WAKORINTHO 5:6b—8
Iondosheni chachu ya zamani, mpate kua donge jipya.
Somo katika barua ya kwanza ya Mtakatifu Paulo kwa Wakorintho
Ndugu zangu: Hamjui kwamba chachu kidogo huchachusha donge lote? Basi, iondosheni chachu ya zamani, mpate kuwa donge jipya, ninyi mlio watu wasiochachuka. Kwa maana mwanakondoo wetu wa Pasaka ametolewa sadaka, ndiye Kristo. Haya, tuadhimishe sikukuu, si kwa chachu ya zamani, wala kwa chachu ya ubaya na uovu, bali kwa donge lisilochachuka, yaani la unyofu na ukweli.
NENO LA BWANA… TUMSHUKURU MUNGU
SEKWENSIA
K. Kristo, Pasaka yetu, amechinjwa sadaka.
Tuile karamuye na twimbe aleluya.
- Aliyejitoa sadaka ya Pasaka
Wakristo wamtolee sadaka ya sifa.
- Mwanakondoo amewakomboa kondoo:
Kristo asiye na dhambi
amewapatanisha na Baba watu wenye dhambi.
- Mauti na uzima vimeshindana ajabu:
Mkuu wa uzima aliyekufa, atawala mzima.
- Utuambie Maria, uliona nini njiani?
Niliona kaburi la Kristo mzima,
na utukufu wa mwenye aliyekufa.
- Mashahidi ni malaika, leso ya uso na mavazi.
Kristo tumaini langu kafufuka: atawatangulia Galilaya.
- Twajua Kristo amefufuka kweli katika wafu:
ewe mfalme mshindaji, utuhurumie. Amina. Aleluya.
SHANGILIO LA INJILI
1 WAKORINTHO 5:7b, 8a
K. Aleluya W. Aleluya.
K. Kristo, Mwanakondoo wetu wa Pasaka, ametolewa sadaka.
Haya, tuadhimishe sikukuu katika Bwana.
W. Aleluya.
INJILI
YOHANE 20:1—9
Imempasa kufufuka katika wafu.
† Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Yohane
Siku ya kwanza ya juma, Maria Magdalena alifika kwenye kaburi asubuhi sana, kungali giza bado, na akaliona jiwe limeondolewa kaburini. Basi akapiga mbio, akafika kwa Simoni Petro na yuel mfuasi mwingine amabaye Yesu alimpenda, akwaambia, “Wamemwondoa Bwana kaburini, na sisi hatujui walikomweka.” Petro akatoka pamoja na yule mfuasi mwingine kwenda kaburini. Wote wawili walipiga mbio, lakini yule mfuasi mwingine alitangulia, maana aalikimbia mbio kuliko Petro, akafika kwanza kwenye kaburi; akainama na kuchungulia, akaviona vitambvaa vya sanda vimelala humo, lakini hakuingia. Simoni Petro akaja nyuma yake, akaingia kaburini, akaviona vitambaa vimelala humo, na kadhalika leso ya kufunikia kichwa chache, hiyo imekunjwa, haikulala pamoja na vitambaa vingine, bali peke yake mahali pake. Hapo Yule mfuasi mwingine aliyefika kwanza kaburini akaingia pia, akaona akasadiki. Kwa maana mpaka hapa walikuwa hawajafahamu bado Maandiko ya kwamba imempasa kufufka katika wafu.
INJILI YA BWANA… SIFA KWAKO EE KRISTO